LILE sakata la walimu wa shule ya
wasichana ya Mtakatifu Fransisco wa Azizi Mbeya (St.Francis) kugomea ndani ya
nyumba limechukuwa sura mpya baada ya Serikali mkoani hapa kuingilia kati
na kuliangukia kanisa Katoliki kutoifunga shule hiyo kama ilivyotarajiwa
baada ya masista wenye asili ya kiasia wa Shirika la Mt.Karoli
Boromeo ambao ndiyo viongozi na waendeshaji wa shule kuitwa mara
moja na mama yao mkuu kurudia haraka nchini Ubelgiji kuhofia
kuvamiwa na walimu hao.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Abbas Kandoro akizungumza katika kikao na
viongozi wa kanisa katoliki Jimbo la Mbeya alichokiitisha ofisini kwake
jana amemsihi Askofu Evaristo Chengula wa kanisa jimbo ambaye ndiye
mmiliki wa shule hiyo kuvuta subira na kubadilisha wazo la kuifunga shule hiyo kwani
serikali imeamua kuingilia katika kulishughulikia suala hilo haraka
iwezekanavyo.
“Tunampa pole Baba Askofu tunajuwa anaumia na
krismas kwake imepita bure,avute subira lakini ajuwe anashughulika na
binadamu aendelee kuwa mvumilivu hasifunge shule…shule hii inatuletea sifa
katika Mkoa na taifa kwa ujumla na kutokana na ubora wa elimu inayotoa
imekuwa ni tegemeo na kimbilio la wengi, wanafunzi zaidi ya 360 wanaosoma
hapo watayumba,wazazi watachanganyikiwa,nawaagiza pande zote mbili na wanasheria
wenu mketi kwa pamoja na kulimaliza suala hili kwa amani na utulivu…ila
siingilii masuala ya kisheria,”alisema.
Hata hivyo Mkuu wa Mkoa Kandoro alituma ujumbe wake ulioongozwa na Mkuu wa
Wilaya ya Mbeya,Evans Balama kwenda kwa Askofu Chengula kufikisha salamu hizo
na kuahidi kulishughulikia tatizo hilo mapema ambapo kwa wake Askofu Chengula
aliiomba serikali kulishughuliki suala hilo kabla ya januari,8 siku ya kufungua
shule za bweni kabla masista hao ambao ndiyo Meneja wa shule hawajaondoka
nchini ili aweze kuwasihi kurejea shuleni vinginevyo ataifunga
shule kutokana na kukosa walimu na Uongozi wa kuiendesha.
Kwa mujibu wa maelezo ya Mkurugenzi wa idara ya elimu Jimbo Katoliki
la Mbeya,Padri Innocent sanga alisema awali masista wa shirika la
Mtakatifu Fancisco wa Asizi waliendesha shule hiyo kwa makubaliano ya mikataba
mizuri na walimu hao kuwalipa mishahara minono iliyofikia
wastani wa Tsh.Mil.2 ,lakini baada ya kumaliza mkataba wao na kuikabidhi shule
kwa Askofu Chengula, Jimbo lilishindwa kuiendesha kutokana na
kutumia fedha nyingi kuwalipa walimu.
“Wenzetu walikuwa na fedha nyingi lakini sisi hatuna chanzo kingine cha
kuendesha shule zaidi ya kutegemea ada kwani shule tunaiendesha
kama huduma na siyo kibiashara,tuliamua kukaa nao kuwaeleza kusudio leo la
kubadilisha mikataba mipya, tuliangalia tunatumia zaidi ya Sh.Mil.548,000,000
kulipa mishahara ya walimu sawa na asilimia 76 ya mapato ya shule na
Sh.Mil176,000,000 sawa na asilimia 24 ndiyo inasalia na tunalazimika
kutumia fedha za gharama ya bweni na chakula ili kufidia mishahara
mikubwa na ndiyo maana ilipofika mwaka huu tulishindwa kabisa kuiendesha
shule”alisema.
Aliongeza,”Askofu aliamua kuwaeleza adhma ya kufuta mikataba mipya ya walimu
wa kudumu,kulipa haki zao zote stahili kwa mujibu wa sheria,kuajiri upya walimu
waliopo na wapya katika mikataba ya muda maalum na masharti mapya ilimradi
yakubaliwe na mwajiri,kufuta marupurupu yote ya walimu ambayo si ya kisheria.
Alitaja marekebisho mengine ya mikataba kuwa kulipa mishahara kadri ya
‘scheme of service and salary structure’ mpya ambayo jimbo limeandaa,kuanzisha
malipo na marupurupu mapya kadri ya uwezo wa shule na kwa mwaka 2011 shule
isipandishe ada kufikia Tsh.Mil.2 kama ilivyokusudia ili kuendelea kuwalipa
walimu miashahara minono na badala yake walimu walipwe wastani wa Sh.600,000 na
ada ibakie Sh.Mil.1.7.
Padre sanga alisema hata hivyo walimu hao hawakuwa tayari kupokea
marekebisho hayo na hivyo kanisa kuamua kuwaachisha kazi na kuwataka
wahame ifikapo Januari,28,2011 ndani ya nyumba za shule walizokuwa
wakiishi kuwapisha walimu wengine wapya walioajiriwa hali ambayo ilipingwa na
walimu hao kwa kuomba hati maalum katika baraza la nyumba kuzuia
wasitokea hadi kesi yao ya msingi iliyopo Tume ya usuluhishi kesi
za ajira na kazi (CMA) itakapomalizika.
Alisema walimu hao pia walipinga kuhama kupitia wakili wao wa
awali Mwakolo and Company kuwa watakuwa tayari kuhama wakati watakapolipwa
madai yao ‘repatrition expenses’,yaani gharama za kuwarudisha makwao ambapo
baada ya kila mmoja kuorodhesha madai yake katika walimu tisa zaidi ya
Sh.Mil.31.9 zilipatikana na kanisa lilikuwa tayari kuwalipa lakini
baadaye waligoma na kuachana na wakili huyo.
Amewataja walimu hao wanaolidai kanisa na idadi ya kiasi cha fedha
katika mabano ni Rozalia Kimario aliyedai zaidi ya Sh.Mil.6.7,Mary Njele
(Sh.Mil.6.6),Yessaya Musyani (Sh.336,000),Lenadina Kagero(Sh.263,000),Ernest
Njole (Sh.332,000),Benezer Msangi (Sh.Mil.6.5),Ursula Ndeki (Sh.Mil.7.5),Agatha
Nyagimba (Sh.328,000) na Simon Mapunda (Sh.Mil.3.2).
Ametaja madai mengine ya walimu ambayo kanisa lilikuwa tayari kulipa
kwa mujibu wa sheria ni pamoja na mshahara wa mwezi mmoja badala ya
notisi ambapo Askofu alikuwa tayari kuwalipa mishahara ya miezi sita,’disturbance
allowances’,’severance allowance’ na ‘Certificate of service cause of
termination(Redundance)’.
“Hapo ndipo ilipoanza mivutano na walimu kulifikisha kanisa katika
baraza la ardhi na nyumba pamoja na Tume ya usuluhishi ambapo ‘order’ ilitolewa
januari,17,2011 walimu walikaa katika nyumba hizo kwa kufuata amri ya baraza la
ardhi na nyumba hadi kesi ilipokwisha disemba,22 ,2011 kesi yao
ilipotupiliwa mbali,na kesi nyingine walimu waliyofungua (CMA)
kuitaka tume itamke kuwa “walimu hao hawakuachishwa kazi kihalali na waendelee
na kazi” ilitupilia mbali pia,”alisema Padri Sanga.
Padri huyo alisema kutokana na maamuzi ya baraza la ardhi na nyumba kanisa
liliiomba kampuni ya Yono auction mart & Cout broker kuwaondoa walimu hao
jambo lililoleta mgongano wa maamuzi baada ya Mwenyekiti wa tume ya usuluhishi
Boniphace Nyambo kuliandikia Jeshi la Polisi hati ya kuwarudisha ndani ya
nyumba majira ya saa 12 jioni jambo lililopelekea kuhoji uhalali wa Tume hiyo
kuandika ‘order’ wakati awali suala la nyumba lilishughulikiwa na
baraza la ardhi na nyumba na kutoa hati iliyokwisha muda wake
baada ya kutupilia mbali shauri hilo.
Alisema Jeshi la polisi liligonga ukuta kupata ufunguo za kuwafungulia
walimu hao ndipo walimu walipochukuwa hatua ya kuvunja makufuli ya nyumba zao
na kuingia ndani ya nyumba hizo kuendelea kuishi hali ambayo iliwashtua masista
ambao nao wanaishi ndani ya shule hiyo na hivyo kuhofia kuvamiwa na walimu na
hivyo kuamua kumpigia simu mama yao mkubwa huko nchini Ubelgiji ambaye aliwataka
waondoke haraka na hivyo walimuaga Askofu Chengula na kuondoka siku ya
pili wakiiacha shule peke yake.
Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi akiwa
safarini kuelekea mkoani Iringa walipo masista wenzao wa Shirika hilo,mmoja wa
viongozi wa masista hao,Sr.Sagaya alisema amesikitishwa na kitendo
kilichofanywa na walimu hao kutishia amani na utulivu na kwamba alilazimika
usiku huo kumpigia simu Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya,Advocate
kumuelezea hali hiyo lakini katika hatua ya kushangaza Kamanda
Nyombi alibariki kitendo hicho na kumuahidi kuwa watakuwa salama na
hakutakuwa na uvunjifu wowote wa amani.
“Sisi tulijiuliza Polisi wanabariki walimu kuvunja nyumba?,lakini pili
tukahoji kama walimu hao wamekaidi kumsikiliza Baba Askofu ambaye ndiyo mwajiri
wao,je watatusikiliza sisi?, watakuja kutuvamia kwa maana zile sauti za nyundo
zilitunyima raha na hamu ya kuendelea kuishi,tukampigia mama mkubwa Ubelgiji
akasema tukimbilie kwa wenzetu Iringa tupo Iringa na amesema hali ikizidi kuwa
mbaya turudi Ubelgiji,”alisema Sr.Sagaya.
Thompson
Mpanji, Redio Maria Mbeya Desemba 28,
2011