UTAFITI wa hivi karibuni uliofanywa katika Chuo Kikuu cha
Tiba cha Johns Hopkins nchini Marekani, umegundua kuwa matumizi ya dawa za
kurefusha maisha (ARV) yanaweza kuwafanya waathirika wa Virusi vya Ukimwi (VVU)
kukutana kimwili na wapenzi wao bila kondomu, pasi kuwapa maambukizi.
Wakati wataalamu hao wakifikia hatua hiyo muhimu katika
kupata jibu la janga hilo
lililoitesa dunia kwa miongo kadhaa sasa, kuna taarifa njema pia za kugunduliwa
kwa chanjo mpya ya Ukimwi.
Kwa upande wa utafiti wa ARV walioufanyiwa majaribio kwenye
sehemu mbalimbali za dunia, umebaini kuwa mtu ambaye anatumia dawa za kurefusha
maisha, anaweza kufanya tendo la ndoa bila ya kutumia kondomu na mtu ambaye
hana Ukimwi na asimwambukize kwa asilimia 95.
Mkuu wa Mtandao wa Maabara za Kuchunguza VVU katika chuo
hicho, Profesa Susan Eshleman, alisema kwenye ripoti ya ugunduzi huo, wamebaini
dawa za kurefusha maisha kwa waathirika wa HIV, sasa zinaweza kutumika kama sehemu ya kuzuia maambukizi.
Profesa Eshleman alisema kwamba muathirika wa VVU anayetumia
ARV kikamilifu anaweza kujamiiana na mtu ambaye hana virusi bila kondomu na
asimwambukize.
“Huu ni ugunduzi wa kustajabisha,” alisema Profesa Eshleman
akifafanua: “Matokea haya yameleta mapambazuko mapya katika sayansi ya kuzuia
maambukizi na inawaweka watafiti kwenye mazingira mazuri zaidi ya kupata
suluhisho la kukabiliana na maradhi haya.”
Walivyogundua njia
Profesa Eshleman anasema utafiti huo walioupa jina la HPTN
052 walifanya kupitia maeneo mbalimbali ya dunia hasa yenye kasi kubwa ya
maambukizi kama vile Afrika, Brazili, India na Thailand.
Kwenye ripoti hiyo ambayo pia ilichapishwa kwenye jarida
maarufu la kisayansi linaloitwa Science, watafiti hao wanasema kwamba mtu
anapotumia ARV, hufikia wakati fulani wingi wa virusi mwilini hupotea kiasi
kwamba anakuwa karibu sawa na yule ambaye hajaambukizwa.
“Jambo la msingi katika utafiti huu ni kwamba dawa hizi za
kurefusha maisha zinapotumiwa kikamilifu, hupunguza mzigo wa virusi mwilini kwa
zaidi ya mara 200. Ni sawa na kusema inapunguza hadi kufikia karibu na sifuri,”
inaeleza ripoti hiyo.
Ni katika mazingira hayo, ripoti hiyo inasema kuwa damu ya
muathirika inakuwa haina virusi na hivyo uwezekano wa kumuambukiza mpenzi wake
unakuwa haupo.
Ripoti hiyo inaeleza kuwa ARV inafanya kazi mbili, kwanza
kurefusha maisha ya muathirika kwa kupunguza virusi mwilini na pili ni kumkinga
asiambukize wengine.
Sifa nyingine ya ARV, anasema ni kwamba inapunguza uwezekano
wa waathirika kupata ugonjwa wa Kifua Kikuu (TB) kutokana na kiwango cha kinga
za mwili kupanda.
Onyo la utafiti
Pamoja na kwamba njia hii imeonekana kuwa ni nzuri kwa ajili
ya kuzuia maambukizi, wataalamu hao wanasema ni hatari pale itakapotumika
vibaya.
Hatari wanayoizungumzia ni kwa muathirika iwapo atatembea na
mpenzi ambaye ni muathirika, lakini akawa hajatumia ARV au ametumia, lakini
siyo kwa kiwango ambacho VVU vimepunguzwa hadi kufikia karibu na sifuri.
Watalaamu hao wanasema iwapo muathirika atapata maambukizo
mapya, atajiweka katika hatari ya kupata usugu kwa aina ya ARV anayotumia.
Ili kuwaweka katika mazingira salama, wataalamu hao
wamewashauri waathirika wanaotumia ARV kutobweteka na badala yake kuendelea
kutegemea kondomu kama moja ya njia za kuzuia
maambukizo mapya na kuimarika kiafya.
Wataalamu wazungumzia utafiti huo
Wataalamu na watafiti mbalimbali wameelezea utafiti huo kuwa
ni mafanikio mazuri katika kurahisisha njia ya chanjo katika kutoa kinga kwa
waathirika na wale ambao hawajaambukizwa.
Kwa sasa zipo aina nane za chanjo za Ukimwi duniani ambazo
wataalamu wapo kwenye hatua mbalimbali za majaribio na wamekuwa wakizielezea
kuwa zina matumaini.
Mkuu wa Mambo ya Afya wa Serikali ya Marekani, Profesa
Anthony Fauci ambaye pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya
Kuambukiza na Mzio (NIAID), aliuelezea ugunduzi huo kuwa ni wakushangaza.
Wataalamu wengine pia wakauelezea kuwa mtu anaweza
kuuchukulia kama ni utani, lakini ni jambo
ambalo litaleta mapinduzi makubwa ya kukabiliana na VVU.
Profesa Eshleman alisema utafiti wao utafungua urahisi wa
njia ya wanasayansi wanaoendelea na tafiti nyingine kuwa katika mazingira
mazuri ya kutatua tatizo hilo.
Profesa Eshleman anasema mkakati walio nao kwa sasa ni
kufanya uchunguzi zaidi wa njia hiyo katika ngazi ya kijamii na kimataifa.
Alisema anaamini kwamba njia hiyo itakuwa na matokeo mazuri
katika ngazi hiyo kabla haijathibitishwa rasmi kutumika kimataifa.
A.Kusini waiwekea mkakati
Serikali ya Afrika Kusini tayari imeweka mkakati wa kutumia
njia hiyo kuliokoa taifa hilo
lenye kasi kubwa ya maambukizo kuliko mengine duniani.
Mmoja wa wataalamu wa afya wa nchi hiyo, Dk Brian Williams,
anasema tayari wamefanya tathmini na kuona baada ya miaka mitano watakuwa
wamefanikiwa kuyakabili maradhi hayo.Dk Willams, anasema Afrika Kusini ina
waathirika milioni sita na kwamba ni asilimia 30 tu wanaopatiwa tiba ya ARV.
“Ili kuwagharimia
waathirika hao itabidi tutumia Dola za Marekani kati ya milioni mbili hadi tatu
(Sh 3.2 trilioni hadi 4.8 trilioni) kununua dawa za ARV kwa mwaka,” alisema Dk
Williams.
Kutokana na uzoefu wake, Williams alisema utafiti huo
utasaidia waathirika kuwa katika mazingira mazuri ya kupatiwa chanjo ambayo ipo
mbioni kupatikana.
Tanzania
ipo pazuri
Tanzania
ni moja ya nchi ambazo matumizi ya ARV kwa waathirika ni makubwa kutokana na
mpango wa Serikali wa kuwapatia dawa hizo bure kote nchini.
Tangu Rais Jakaya Kikwete atangaze mpango wa kupima kwa
hiari miaka michache baada ya kuingia madarakani, aliwahakikishia wale wote
watakaojikuta wameambukizwa, watapatiwa dawa za kurefusha maisha bure.
Mwananchi Jumapili lilipowasiliana kwa njia ya simu na
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda, alisema asingeweza
kulizungumzia suala hilo kwa kuwa hakuwa ofisini na asingependa kuzungumza kwa
njia ya simu.
Mkuu wa Utawala wa Taasisi ya Utafiti wa Tiba ya Binadamu
Hospitali ya KCMC (KCRI), Lucy Shara alilimbia gazeti hili kwamba suala la
matumizi ya ARV nchini imekuwa ikifanyika ipasavyo kwa wale wanaojitokeza kwa
hiari.
Shara alikiri kuwa wataalamu nchini wamekuwa kwenye tafiti
mbalimbali za VVU na kwamba hata suala la ufanisi wa dawa za ARV wamekuwa
wakiujadili mara kwa mara kupitia vikao na semina mbalimbali.
Lakini akasema suala la utafiti huo wa Marekani lilijadiliwa
kwenye mkutano uliofanyika Jijini Dar es Salaam karibuni.
“Juzi tulikuwa kwenye semina hapo Dar es Salaam. Wasiliana
na wataalamu wetu wa pale Muhimbili (Hospitali ya Taifa) wanaweza wakakueleza
jambo hili kwa uzuri zaidi,” alisema Shara.
Juhudi za kuwapata wataalamu wa Utafiti wa Chuo Kikuu cha
Tiba na Sayansi Muhimbili (MUHAS) kulieleza suala hili hazikufanikiwa kutokana
na tatizo la kimawasiliano.
Chanjo mpya yagundulika
Utafiti wa chanjo Ukimwi uliosimamiwa na Chuo Kikuu cha Tiba
cha Harvard nchini Marekani na kusimamiwa na Profesa Dan Barouch wa chuo
unaelezewa kuwa na mafanikio makubwa katika kukabiliana na ugonjwa wa Ukimwi
ambao mpaka sasa hauna chanjo wala tiba ambayo imetambuliwa rasmi kimataifa.
Taarifa iliyotolewa NIAID kwa gazeti hili wiki iliyopita,
inaeleza kuwa utafiti huo uliofanywa Profesa Nelson Michael wa Jeshi la
Marekani, akishirikiana na Profesa Jaap Goudsmit, Dk Vanessa Hirsch na Ilnour
Ourmanov, una sema mafanikio ya utafiti huo yanawapa matumaini ya kupata chanjo
madhubuti.
Walisema kwenye ripoti hiyo kuwa katika majaribio kadhaa
waliyofanya, chanjo hiyo iliweza kumsaidia Nyani kuwa na chembechembe kinga
ambazo zina uwezo wa kumkinga asiweze kuambukizwa VVU.
Utafiti huo uliotangazwa Januri 4, mwaka huu unaeleza kuwa
kinachofanyika kwa sasa ni kuendelea na utafiti huo katika hatua ya majaribio kwa
binadamu.Kwa sasa chanjo hiyo walisema ipo kwenye hatua ya awali ya majaribio
ya usalama wa dawa kabla ya kuingia kwenye majaribio ya uwezo wa dawa kwenye
mwili wa bianadamu.
Utafiti ulivyofanyika
Walisema walimpa nyani chanjo hiyo na baada ya muda alitengeneza
chembechembe kinga za aina ya protini na walipojaribu kumuambukiza VVU, virusi
walidhibitiwa na kushindwa kushambulia seli nyeupe za binadamu ama kwa jina la
kitaalamu CD4, ambazo ni kinga muhimu dhidi ya maradhi mengine.
Kwa kawaida VVU hushambulia seli hizi nyeupe na kuzifanya
makoloni ya kuwawezesha kuzaliana na kuongezeka mara dufu mwilini hivyo kujenga
mazingira ya mtu kuugua Ukimwi.
Matokeo ya utafiti huo yanafikisha idadi ya aina nane za
chanjo dhidi ya VVU ambazo zimo kwenye majaribio katika hatua mbalimbali
duniani.
Mojawapo ya chanjo hizo amabazo zipo kwenye hatua mbalimbali
za majaribio, ipo ile ambayo mafanikio makubwa yalichangiwa na wanasayansi wa
hapa nchini waliokuwa wanafanya kazi katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC, mkoani
Kilimanjaro.
Wanasayansi wa Tanzania waligundua kwamba baadhi ya watu
walioathirika na Virusi vya Ukimwi (VVU), kwa muda fulani wanajijengea wenyewe
kinga inayoweza kudhibiti virusi hivyo na kuwa na afya njema bila kuwa na haja
ya kutumia dawa za ARV.
Wataalamu hao wa KCMC mjini Moshi walifanikisha utafiti huo
wa mwaka 2006 na 2010 na mwishoni mwa mwaka jana wakaliambia Mwananchi Jumapili
kuhusu ugunduzi huo.
Kiongozi wa Ushirikiano wa kiutafiti kati ya KCMC na Chuo
Kikuu cha Afya cha Duke cha nchini Marekani, Dk Elizabeth Reddy aliliambia
gazeti hili kuwa matokeo hayo yatawezesha kutengeneza chanjo itakayowezesha
watu wote kuwa na kinga hizo, hivyo kutoathirika na VVU.
Alisema jambo la msingi katika utafiti huo ni kugundulika
kwa VVU kuwa wana gamba lenye protini iliyochanganyika na sukari, ambayo
huvifanya kushindwa kutambuliwa na kinga za kawaida za mwili wa binadamu.
Lakini, Dk Reddy alisema kuwa katika ugunduzi wao, wamebaini
aina ya kinga za mwili ambazo hutambua virusi kupitia aina hiyo ya sukari kwenye
gamba la nje la VVU na kuvishambulia hadi kuviua.
Alisema kuwa utafiti huo ulifanyika katika maabara ya KCMC
kwa ushirikiano wa timu ya wataalamu wa afya wa Tanzania pamoja na wa Marekani.
Alibainisha kuwa utafiti huo ulihusisha Watanzania kadhaa walioambukizwa
VVU hapa nchini, lakini wamekuwa wakiishi bila kuathirika.
Dk Reddy alisema
kuwa utafiti huo umefanyika maeneo mengi duniani, lakini kituo cha KCMC ndicho
kilichotoa mwanga mkubwa zaidi ambao hatua zake za mwisho zilithibitishwa na
wataalamu waliobobea nchini Marekani.
Kiongozi huyo wa utafiti, alisema kuwa Taasisi ya Utafiti wa
Magonjwa inayosimamiwa na Mfuko wa Good Samaritani (GSF) ambao ndio pia
unaosimamia taasisi nyingine kama vile Chuo Kikuu cha Afya cha Tumaini na
Hospitali ya KCMC, ndiyo inayopaswa kupewa shukurani kwa matokeo hayo.
Dk Reddy anaamini kwamba ndani ya kipindi cha miaka mitano
ijayo, chanjo kadhaa zitakuwa zimethibitishwa.
hatari kweli kweli ka ndio hivyo
ReplyDelete