Wakati jeshi la Sudan likisema kiongozi huyo wa waasi, Khalil Ibrahim,
aliuwawa katika mapambano akijaribu kuingia kisiri hadi Sudan Kusini
wiki iliyopita, kundi la waasi la JEM lilipinga, likisema aliuwawa
katika shambulizi la angani, na kudai nchi za magharibi zilihusika
katika shambulizi hilo.
Gazeti la Sudan Tribune lilinukuu taarifa ya kundi la JEM iliyosema
tukio hilo linaashiria ushirikiano na njama ya baadhi ya nchi za eneo
hilo na kimataifa na serikali ya mauaji ya kimbari katika jimbo la
Darfur.
Kulingana na msemaji wa kundi hilo, ambalo lilijiondoa kitoka
mpango wa amani na serikali mwaka jana, amesema kwa kufanya njama hiyo,
serikali ya Sudan imefungua milango ya mauaji ya kisiasa.
Ibrahim yadaiwa alirejea kutoka nchini Libya mwaka huu, baada ya
kuanguka kwa utawala wa Muammar Gaddafi, ambapo kundi la JEM lilipata
msaada. Taifa jipya huru la Sudan Kusini pia linashtumiwa na serikali ya
Sudan kwa kuwasaidia waasi.
Kulingana na ripoti na mikanda ya video inayoenezwa kwenye mitandao ya
internet, polisi mjini Khartoum waliwatawanya wafuasi wa JEM waliojaribu
kutoa rambirambi zao nyumbani kwa familia ya Ibrahim viungani mwa mji
huo mkuu wa Sudan. Haijabainika ni nani atakayechukua mahala pa kiongozi
wa kundi hilo la waasi ambalo aliliunda mwaka 2000.
#b#Katika mzozo wa Darfur, ambao umeendelea tangu mwaka 2003, zaidi ya
watu laki tatu wameuwawa kulingana na Umoja wa mataifa, ijapokuwa
serikali ya Sudan inasema idadi hiyo iko chini.
Waziri wa habari wa Sudan, Abdullah Massar, amesema kifo cha Ibrahim
kinatuma ujumbe kwa makundi ya waasi kuisikia sauti ya busara na
kujiunga na mchakati wa kutafuta amani. Alisema jana kuwa milango yao
iko wazi na kwamba mkataba wa Doha ungali wazi.
Kifo cha Ibrahim, ambaye kila mara alitajwa kuwa kiongozi jasiri,
huenda kikawa pigo kubwa kwa kundi la waasi wa JEM. Mtalaamu mkuu nchini
Sudan, Alex de Waal, amesema Khalil Ibrahim alitawala kundi la JEM na
kibinafsi alibaini mikakati ya kisiasa na kijeshi ya kundi hilo na hasa
ndiye aliyezuia kundi hilo kufanya mazungumzo ya amani na serikali ya
Sudan, hivyo kifo chake ni pigo kubwa kwa waasi hao.
Uongozi katika mji mkuu wa Khartoum utahisi kukichukulia kifo chake kwa
kuzingatia kuwa uasi katika jimbo la Darfur sasa umekwisha. Wakati
tishio linalotolewa na kundi la JEM bila shaka likionekana kupungua,
inaweza kuwa makosa kwa serikali kudhani kuwa mgogoro wa kisiasa katika
jimbo la Darfur unaweza kutatuliwa kwa urahisi.
No comments:
Post a Comment