Wednesday, December 28, 2011

KIM JONG IL AZIKWA

Kiongozi mpya wa Korea Kaskazini anaongoza msafara wa mazishi ya baba yake Kim Jong Il, ambao unapita katika mitaa ya mji mkuu wa Pyongyang uliofunikwa na barafu na theluji. Picha za Televisheni ya taifa ya Korea Kaskazini zimemuonyesha Kim Jong Un akitembea sambamba na gari lililobeba jeneza la baba yake. 

Gari jingine lililobeba picha kubwa ya hayati Kim Jong Il lilifuatia katika msafara huo. Maelfu ya waombolezaji wamejipanga kando kando ya barabara wakivumilia baridi kali kumuaga kiongozi wao, na wanajeshi wanainamisha vichwa vyao kutoa heshima. 

Kim Jong Il alikufa kutokana na mshituko wa moyo mapema mwezi huu, na mazishi yake yatachukua muda wa siku mbili. Mara tu baada ya kifo chake, vyombo vya habari viliashiria kwamba Kim Jong Un ndiye atakayerithi madaraka ya baba yake.

No comments:

Post a Comment