Tuesday, December 27, 2011

SUGU ATOA MSAADA KWA WAATHIRIKA WA MAFURIKO MBEYA

WANANCHI waliokumbwa na mafuriko Desemba 19 mwaka huu katika Mtaa wa Ikuti Jijini Mbeya na kusababisha kifo cha watoto wawili,  juzi wamepata msaada wa mahindi gunia 40 kutoka kwa Mbunge wa Jimbo hilo Joseph Mbilinyi (Sugu)(Chadema).

Mbunge huyo alikabidhi msaada huo kwa Afisa Mtendaji wa Kata ya Iyunga, Adia Mwambela chini ya uangalizi wa Mwenyekiti wa Chama cha Msalaba Mwekundu mkoa wa Mbeya Ulimboka Mwakilili ambaye alikabidhiwa jukumu la kuwagawia walengwa wa msaada huo.

Sugu alisema baada ya kusikia taarifa za mafuriko hayo akiwa nje ya mkoa, hakupenda kutoa matamko akiwa mbali na badala yake akaamua kurudi jimboni kujionea hali halisi na kusikiliza mahitaji ya wahanga na ndicho kilichomgusa kutoa msaada huo wa mahindi.

Alisema baada ya kuwatembelea wahanga wa mafuriko hayo, kwa kauli yao wenyewe walidai kuwa hitaji lao la kwanza ni chakula, kwa kuwa akiba waliyokuwa nayo ilisombwa na maji.

Sanjari na hilo alitanabaisha kuwa kwasababu yeye ni mwanamuziki, aliamua kufanya tamasha la Muziki siku ya mkesha wa krismasi, ambapo aliahidi kuwa katika kila tiketi ya kiingilio kwenye tamasha hilo iliyouzwa kwa shilingi 3000, shilingi 1000 itaelekezwa kusaidia wahanga wa mafuriko hayo.

Alisema kuwa katika tamasha hilo tiketi 1200 ziliuzwa na kufanikisha kukusanywa kwa shilingi milioni 3.6 na theluthi ya fedha hizo ikaelekezwa kwa wahanga hao kama alivyoahidi.

“Baada ya kukusanya fedha hizi hatukuona sababu yoyote ya kukodi fuso kwenda kununua mahindi sehemu nyingine nje ya eneo hili hapa wakati kuna akina mama na shangazi zetu wanauza mahindi hapa, hivyo tumeamua fedha hizi zibaki hapa hapa ili zisaidie kukuza uchumi wa eneo hili,” alisema Mbilinyi.

Pia aliwashukuru wananchi wa maeneo hayo ambao hawakukumbwa na athari za mafuriko hayo kwa kujitolea kuwasaidia wenzao walioathiriwa nyumba na mali zao kwa kuwasaidia kuokoa mali na kuwapa hifadhi wale ambao nyumba zao zilibolewa kabisa.

Afisa Mtendaji wa Kata ya Iyunga, Adia Mwabela alimshukuru mbunge huyo na kudai kuwa ameonyesha mfano bora kwa viongozi wengine pia kujitokeza na kusaidia wahanga wa mafuriko hayo.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Msalaba Mwekundu Mkoa wa Mbeya, Ulimboka Mwakilili alisema msaada huo utawafikia walengwa kama ilivyokusudiwa na kuwa ugawaji wa msaada huo hauzingatii itikadi ya chama chochote wala kuingiliwa na Serikali.

Alisema mbali na msaada huo wa Mbunge, taasisi za dini za Kiislam na Kikristo zimejitokeza kutoa misaada ya kiutu huku Serikali kuu na Jiji la Mbeya pia wakiwa mstari wa mbele kutoa misaada hiyo lakini wafanya biashara pekee hawajajitokeza huku wakishindwa kujua kuwa walioathirika ni wateja wake.

Imeandikwa na Gordon Kalulunga Kalulunga Community Group Desemba 27, 2011

No comments:

Post a Comment