Wednesday, December 28, 2011

SAKATA LA WALIMU WA ST. FRANCIS MBEYA LACHUKUA SURA

LILE sakata la walimu wa shule ya wasichana ya Mtakatifu Fransisco wa Azizi Mbeya (St.Francis) kugomea ndani ya nyumba  limechukuwa sura mpya baada ya Serikali mkoani hapa kuingilia kati na kuliangukia kanisa Katoliki kutoifunga shule hiyo  kama ilivyotarajiwa  baada ya masista wenye asili ya kiasia wa Shirika la Mt.Karoli  Boromeo  ambao ndiyo viongozi na waendeshaji wa shule kuitwa mara moja na mama yao mkuu  kurudia haraka nchini Ubelgiji  kuhofia  kuvamiwa na walimu hao.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Abbas Kandoro akizungumza katika kikao  na viongozi wa kanisa katoliki Jimbo la Mbeya  alichokiitisha ofisini kwake jana amemsihi Askofu Evaristo Chengula wa kanisa jimbo  ambaye ndiye mmiliki wa shule hiyo kuvuta subira na kubadilisha wazo la kuifunga shule hiyo kwani serikali imeamua kuingilia katika  kulishughulikia suala hilo haraka iwezekanavyo.

“Tunampa pole Baba  Askofu  tunajuwa anaumia  na  krismas kwake imepita bure,avute subira  lakini ajuwe anashughulika na binadamu aendelee kuwa mvumilivu hasifunge shule…shule hii inatuletea sifa katika Mkoa na taifa kwa ujumla  na kutokana na ubora wa elimu inayotoa imekuwa ni tegemeo na kimbilio la wengi, wanafunzi  zaidi ya 360 wanaosoma hapo watayumba,wazazi watachanganyikiwa,nawaagiza pande zote mbili na wanasheria wenu mketi kwa pamoja na kulimaliza suala hili kwa amani na utulivu…ila siingilii masuala ya kisheria,”alisema.

Hata hivyo Mkuu wa Mkoa Kandoro alituma ujumbe wake ulioongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya,Evans Balama kwenda kwa Askofu Chengula kufikisha salamu hizo na kuahidi kulishughulikia tatizo hilo mapema ambapo kwa wake Askofu Chengula aliiomba serikali kulishughuliki suala hilo kabla ya januari,8 siku ya kufungua shule za bweni  kabla masista hao ambao ndiyo Meneja wa shule hawajaondoka nchini ili aweze kuwasihi  kurejea shuleni  vinginevyo ataifunga shule kutokana na kukosa  walimu na Uongozi wa   kuiendesha.

 Kwa mujibu wa maelezo ya Mkurugenzi wa idara ya elimu Jimbo Katoliki la Mbeya,Padri  Innocent sanga alisema  awali masista wa shirika la Mtakatifu Fancisco wa Asizi waliendesha shule hiyo kwa makubaliano ya mikataba mizuri na  walimu hao  kuwalipa mishahara  minono iliyofikia wastani wa Tsh.Mil.2 ,lakini baada ya kumaliza mkataba wao na kuikabidhi shule kwa Askofu Chengula,  Jimbo lilishindwa kuiendesha  kutokana na  kutumia fedha nyingi kuwalipa walimu.

“Wenzetu walikuwa na fedha nyingi lakini sisi hatuna chanzo kingine cha kuendesha shule zaidi ya kutegemea ada  kwani  shule tunaiendesha kama huduma na siyo kibiashara,tuliamua kukaa nao kuwaeleza kusudio leo la kubadilisha mikataba mipya, tuliangalia tunatumia zaidi ya Sh.Mil.548,000,000 kulipa mishahara ya walimu sawa na asilimia 76 ya mapato ya shule na Sh.Mil176,000,000 sawa na asilimia 24 ndiyo inasalia  na tunalazimika kutumia fedha za gharama ya bweni na chakula ili kufidia mishahara mikubwa  na ndiyo maana ilipofika mwaka huu tulishindwa kabisa kuiendesha shule”alisema.

Aliongeza,”Askofu aliamua kuwaeleza adhma ya kufuta mikataba mipya ya walimu wa kudumu,kulipa haki zao zote stahili kwa mujibu wa sheria,kuajiri upya walimu waliopo na wapya katika mikataba ya muda maalum na masharti mapya ilimradi yakubaliwe na mwajiri,kufuta marupurupu yote ya walimu ambayo si ya kisheria.

Alitaja marekebisho mengine ya mikataba  kuwa kulipa mishahara kadri ya ‘scheme of service and salary structure’ mpya ambayo jimbo limeandaa,kuanzisha malipo na marupurupu mapya kadri ya uwezo wa shule na kwa mwaka 2011 shule isipandishe ada kufikia Tsh.Mil.2 kama ilivyokusudia ili kuendelea kuwalipa walimu miashahara minono na badala yake walimu walipwe wastani wa Sh.600,000 na ada ibakie Sh.Mil.1.7.

Padre sanga alisema hata hivyo walimu hao hawakuwa tayari kupokea marekebisho hayo  na hivyo kanisa kuamua kuwaachisha kazi na kuwataka wahame  ifikapo Januari,28,2011 ndani ya nyumba za shule walizokuwa wakiishi kuwapisha walimu wengine wapya walioajiriwa hali ambayo ilipingwa na walimu hao kwa  kuomba hati maalum  katika baraza la nyumba kuzuia wasitokea hadi kesi yao ya msingi iliyopo Tume ya usuluhishi   kesi za ajira na kazi (CMA) itakapomalizika.

Alisema walimu hao  pia walipinga kuhama  kupitia wakili wao wa awali Mwakolo and Company kuwa watakuwa tayari kuhama wakati watakapolipwa madai yao ‘repatrition expenses’,yaani gharama za kuwarudisha makwao ambapo baada ya kila mmoja kuorodhesha madai yake katika walimu tisa zaidi ya Sh.Mil.31.9 zilipatikana na  kanisa lilikuwa tayari kuwalipa lakini baadaye waligoma na kuachana na wakili huyo.

Amewataja walimu hao wanaolidai kanisa  na idadi ya kiasi cha fedha katika mabano ni Rozalia Kimario aliyedai zaidi ya Sh.Mil.6.7,Mary Njele (Sh.Mil.6.6),Yessaya Musyani (Sh.336,000),Lenadina Kagero(Sh.263,000),Ernest Njole (Sh.332,000),Benezer Msangi (Sh.Mil.6.5),Ursula Ndeki (Sh.Mil.7.5),Agatha Nyagimba (Sh.328,000) na Simon Mapunda (Sh.Mil.3.2).

Ametaja madai mengine ya walimu ambayo kanisa  lilikuwa tayari kulipa kwa mujibu wa sheria ni pamoja na mshahara wa mwezi mmoja  badala ya notisi ambapo Askofu alikuwa tayari kuwalipa mishahara ya miezi sita,’disturbance allowances’,’severance allowance’ na ‘Certificate  of service cause of termination(Redundance)’.

“Hapo ndipo ilipoanza mivutano na walimu kulifikisha kanisa  katika baraza la ardhi na nyumba pamoja na Tume ya usuluhishi ambapo ‘order’ ilitolewa januari,17,2011 walimu walikaa katika nyumba hizo kwa kufuata amri ya baraza la ardhi na nyumba hadi kesi  ilipokwisha disemba,22 ,2011 kesi yao ilipotupiliwa mbali,na kesi nyingine  walimu waliyofungua  (CMA) kuitaka tume itamke kuwa “walimu hao hawakuachishwa kazi kihalali na waendelee na kazi”  ilitupilia mbali pia,”alisema Padri Sanga. 

Padri huyo alisema kutokana na maamuzi ya baraza la ardhi na nyumba kanisa liliiomba kampuni ya Yono auction mart & Cout broker kuwaondoa walimu hao jambo lililoleta mgongano wa maamuzi baada ya Mwenyekiti wa tume ya usuluhishi Boniphace  Nyambo kuliandikia Jeshi la Polisi hati ya kuwarudisha ndani ya nyumba majira ya saa 12 jioni jambo lililopelekea kuhoji uhalali wa Tume hiyo kuandika  ‘order’  wakati awali suala la nyumba lilishughulikiwa na   baraza la  ardhi na nyumba na kutoa hati iliyokwisha muda wake baada ya kutupilia mbali shauri hilo.

Alisema  Jeshi la polisi liligonga ukuta kupata ufunguo za kuwafungulia walimu hao ndipo walimu walipochukuwa hatua ya kuvunja makufuli ya nyumba zao na kuingia ndani ya nyumba hizo kuendelea kuishi hali ambayo iliwashtua masista ambao nao wanaishi ndani ya shule hiyo na hivyo kuhofia kuvamiwa na walimu na hivyo kuamua  kumpigia simu mama yao mkubwa huko nchini Ubelgiji ambaye aliwataka waondoke haraka na hivyo walimuaga Askofu Chengula na kuondoka  siku ya pili wakiiacha shule peke yake.

 Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wa habari hizi akiwa safarini kuelekea mkoani Iringa walipo masista wenzao wa Shirika hilo,mmoja wa viongozi wa masista hao,Sr.Sagaya alisema amesikitishwa na kitendo kilichofanywa na walimu hao kutishia amani na utulivu na kwamba alilazimika usiku huo  kumpigia simu Kamanda wa polisi Mkoa wa Mbeya,Advocate kumuelezea hali hiyo   lakini katika hatua ya kushangaza Kamanda Nyombi  alibariki kitendo hicho na kumuahidi kuwa watakuwa salama na hakutakuwa na uvunjifu wowote wa amani.

“Sisi tulijiuliza Polisi wanabariki walimu kuvunja nyumba?,lakini pili tukahoji kama walimu hao wamekaidi kumsikiliza Baba Askofu ambaye ndiyo mwajiri wao,je watatusikiliza sisi?, watakuja kutuvamia kwa maana zile sauti za nyundo zilitunyima raha na hamu ya kuendelea kuishi,tukampigia mama mkubwa Ubelgiji akasema tukimbilie kwa wenzetu Iringa tupo Iringa na amesema hali ikizidi kuwa mbaya turudi Ubelgiji,”alisema Sr.Sagaya.
Thompson Mpanji,  Redio Maria Mbeya Desemba 28, 2011

No comments:

Post a Comment